Friday, March 30, 2012

Tibaigana kuihukumu Yanga leo

KAMATI ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Soka Tanzania TFF chini ya Mwenyekiti  Alfred Tibaigana, leo inategemewa kutoa hukumu ya wachezaji wa Yanga waliomshambulia mwamuzi Israel Nkongo kwenye mchezo dhidi ya Azam.

Kamati hiyo wiki iliyopita iliwashangaza wengi baada ya kusimamisha adhabu kwa wachezaji  wa Yanga kwa madai Kamati ya Ligi iliyotoa adhabu ya kuwafungia wachezaji hao haikuwa na mamlaka ya kufanya hivyo.

Akizungumza jijini jana, Ofisa habari wa TFF, Boniface Wambura alisema kamati ya Tibaigana ilikutana jana jioni mara baada ya kuwasilishwa kwa rufani ya Yanga na kusikilizwa hivyo maamuzi juu ya wachezaji hao itatolewa leo.

Alisema mara baada ya Kamati ya Nidhamu kusimamisha adhabu za wachezaji hao walipewa muda wa wiki mbili kuhakikisha wanawasilisha maamuzi ya Kamati yaLigi pamoja na rufaa iliyokatwa na Yanga kupinga adhabu hiyo.

"Kikao cha Kamati ya Nidhamu kinakutana leo jioni (jana)baada ya kukamilisha utaratibu wote ikiwemo kupeleka rufaa ya Yanga waliyokata kupinga adhabu yao pamoja na maamuzi ya kamati ya ligi iliyowafungia wachezaji wa Yanga mara baada ya kikao hicho maamuzi ya mwisho juu ya wachezaji hao itatolewa," alisema Wambura.

Wachezaji wa Yanga waliofungiwa na hatimaye kufunguliwa kwa muda ni Stephano Mwasika (mwaka moja), Jerryson Tegete (miezi sita), Nadir Haroub (mechi sita), Omega Seme na Nurdin Bakari walifungiwa kila moja mechi tatu na wote walitakiwa kulipa fidia kwa kitendo chao hicho cha kumshambulia mwamuzi.

Wakati huo huo; Mabingwa hao watetezi, Yanga tayari wamewasili jijini Tanga kujiandaa na mchezo wao wa kesho wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Akizungumza na gazeti hili, Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa alisema kikosi hicho kimeondoka Dar es Salaam na wachezaji wote pamoja na wale waliokuwa wamefungiwa na kufunguliwa.

Mwesigwa alisema Kamati ya Tibaigana ni kamati huru hivyo hakuna sababu ya kuwaacha au kuogopa kuwachezesha wachezaji waliofungiwa kwa kuwa adhabu yao imesimamishwa kwa muda wa siku 14 ambazo bado hazijakwisha.

Naye kocha Kostadin Papic alisema kikosi chake kipo imara kwa ajili ya mchezo huo huku akiwe wazi kuhusu suala la kuwatumia nyota wake wanaosubiri hukumu leo.

Papic alisema ikibidi watacheza ingawa hafikirii kama watacheza kwa kiwango chao kwa kuwa walishakata tamaa ya kucheza hivi karibuni.

"Kwenye mazoezi wamefanya vizuri baada ya kufunguliwa kwa muda, lakini siamini kama watacheza kwa ari kwa kuwa walishakata tamaa, ila ikibidi kuwatumia nitawatumia,"alisema Papic.

Posted by Raymond Edson

No comments:

Post a Comment