Sunday, April 15, 2012

BARAZA LA HABARI TANZANIA( MCT)LAKEMEA HABARI ZINAZOMHUKUMU MSICHANA LULU KUWA AMEMUUA KANUMBA




April 13, 2012 kamati ya maadili ya maadili ya baraza la habari tanzania MCT, imesikitishwa na ukiukwaji mkubwa wa maadili uliojitokeza hivi karibuni kwa baadhi ya vyombo vya habari ambavyo  wakati vikiripoti kuhusu kifo cha msanii kanumba, vimemhukumu msichana Elizabeth Michael Kimemeta maarufu kama Lulu , kuwa amemuua msanii huyo.

Ukiukwaji huo umejitokeza hasa baada ya msichana huyo kufikishwa mahakamani, ambapo baadhi ya magazeti yanayoheshimika katika jamii yaliandika vichwa vikubwa vinavyosema: LULU KORTINI KWA KUMUUA KANUMBA, NA LULU KIZIMBANI KWA MAUAJI YA KANUMBA.

Kwa mujibu wa sheria na maadili ya uandishi  habari mtu yeyote anayekamatwa kwa tuhuma yoyote ni mtuhumiwa mpaka atiwe hatiani na mahakama, Baraza pia limeshatoa matamko mara kadhaa kuwakumbusha wana habari kujiepusha na uandishi wa habari au vichwa vya habari vinavyohukumu.
Baraza linafahamu fika kuwa kesi zilizoko mahakamani ni kivutio kwa umma, kutaka kujua kinachoendelea ili kuona haki ikitendeka na pia wanahabari wana haki ya kujua na kuripoti yanayojiri huko na katika vyombo vingine vya sheria.

Ni wazi kuwa vichwa vya habari vilivyotajwa hapo juu vimeingilia uhuru wa mahakama kwa kuchapisha habari ambazo zinaonekana kushawishi na kushinikiza uamuzi wa mahakama.
Baraza la habari linawakumbusha wahariri kuhakikisha kuwa wanafanya kazi yao kwa kuzingatia maadili, na weledi katika kuripoti mkasa huu unaogusa hisia za watu.

                                                                     Imetolewa na jaji 
Thomas B. Mihayo
 Mwenyekiti, kamati ya maadili ya baraza la habari Tanzania



POSTED BY MADUHU SALOME



No comments:

Post a Comment